Friday 27 April 2012

Mifumo ya uchumi wa kiIslam No 2

Kuna mifumo ya kiuchumi tofauti tofauti ambayo inatumiwa na bank za kiislam kwa ajili ya kufikia malengo yake mbalimbali kama vile kutoa huduma muhimu kwa wateja, kujipanua katika biashara zake na mengineyo. Makala hii itaelezea kwa mukhtasari mifumo shirikishi (Participatory), mifumo isiyokua shirikishi (Non-participatory) na mifumo upitishaji (Accessory).

Mfumo Shirikishi unatumika pale wahusika watakaposhirikiana katika biashara Fulani. Katika mfumo huu bank za kiislam zinatumia utaratibu unaojulikana Kama Mudaraba au musharaka (partnership). Mudaraba maana yake ni ushirikiano ambao mmoja ya washirika anatoa mtaji (capital) kama vile pesa, na mshirika mwengine anatoa juhudi zake kama vile elimu aliyonayo na kadhalika. Washirika wa aina hii watakubaliana kutokana na wanavyotaka ilimradi tu wasivunje sheria. Kisheria Makubaliano hayo yanatakiwa yawe kabla ya kuanza biashara husika, wakifanya hivyo basi watashirikiana pia katika faida itakayopatikana. kama itapatikana hasara basi yule aliyetoa mtaji (capital) ndie atakaepata hasara ya mtaji na yule aliyetoa juhudi atakua amepoteza kuhudi zake na wakati wake. Hapa yanaweza kujitokeza maswali mengi kama vile nini hukumu ya kisheria kama mmoja wa washirika hao atasababisha hasara kwa uzembe? hilo litazungumziwa kwa ufasaha zaidi hapo baadae.

Aina nyengine ya mfumo shirikishi ni musharaka (Profit and Loss Sharing) ambayo maana yake ni washirika katika biashara fulani watakaposhirikiana katika hali zote katika biashara yao, kwa mfano kila mshiriki atatoa mtaji (capital) na pia akatoa juhudi ktk kuendesha biashara yao isipokua kama kuna makubaliano maalumu. Washiriki hawa watagawana faida na hasara kiasi walivyoshirikiana na walivyokubaliana.

Mfumo usio shirikishi (Non-Participatory) ni mfumo ambao bank sio mshirika katika biashara husika, inamuachia mteja kufanya kila kitu yeye mwenyewe. Ktk mfumo huo aina za biashara zinazotumika ni kama vile Murabaha, salam na Istisnaa. Murabaha (cost plus profit financing) ni pale bank itakaponunua bidhaa kwa makubaliano na mteja na baadae bank ikamuuzia bidhaa hiyo wakati imeshaongeza faida yake. Moja ktk masharti ya murabaha ni pamoja na bank kutaja thamani iliyonunulia bidhaa hiyo.

Salam ni pale thamani ya bidhaa itakapotolewa wakati bidhaa hiyo haipo au haijawa tayari. Istisnaa ni kutoa thamani ya bidhaa zinazohusiana na viwanda(manufuctures) wakati bidhaa hizo hazijawa tayari. Ikumbukwe kwamba biashara aina ya Salam na Istisnaa zinatumika katika mazingira yasiyokua ya kawaida, kwani katika mazingira ya kawaida kinachouzwa kinatakiwa kiwepo wakati wa kuuziana. Lakini hata hivyo hili limeruhusiwa ndani ya Quraan, Hadithi na Ijmaa (consensus) kwa ajili ya kuwafanyia wepesi binadamu, pale tu yatakopokamilika masharti yafuatayo 1- Nilazima bei ya bidhaa ijulikane kwawahusika 2- wakati na mahali pakukabidhiana lazima pajulikane wakati wakufunga mikataba.

Upitishaji (Accessory or Miscellaneous) ni mfumo mwengine unaokubalika kiIslam. Katika mfumo huu bank inachukua malipo ya kazi yake tu, aina za biashara inayotumika katika mfumo huu ni kama Uwakala (agency), mfano wake ni pale bank inapochaguliwa kwa kazi maalumu kama vile uwakala wa kuuza au kununua zabuni fulani. Mara nyengine bank inatumika kama amanah (trustee) maana yake ni kwamba bank inachaguliwa kua msimamizi tu wa biashara au mkataba fulani.

Bank hiyo hiyo inaweza kufanya kazi ya uhamishaji tu hii inaitwa Hawalah (transfer) maana yake nipale bank inaposimamia uhamishaji wa umiliki kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine. Kwa maelezo zaidi fuatilia makala zijazo.

No comments:

Post a Comment