Saturday 24 November 2012

Uwakala (agency)

Ili kufanya maisha yawe mepesi sheria ya kiIslam imeruhusu kitu kinachoitwa wakala (agency).

Wakala maana yake ni mtu au kikundi fulani kufanya kitu fulani kwa niaba ya mtu au kikundi kingine. Wakala ni neno la kiarabu ambalo waarabu wanalitumia kwa maana hiyo hiyo kama linavyotumika katika lugha ya Kiswahili.
Katika sheria wakala maana yake ni mkataba maalum ambao mtu au kundi fulani linafunga na mtu au kundi jengine kwa kufanya kazi zake kama ambavyo angezifanya yeye mwenyewe. Kwa mfano A atakapo mwambia B ninunulie gari mbili kutoka Japan, katika mfano huu B anachukua nafasi ya A katika haki Fulani Fulani atakazopewa na A, tunasema haki Fulani Fulani kwa sababu B anatakiwa afanye yale tu atakayoruhusiwa na A.

Kutokana na mfano huo hapo juu inawezekana pia mteja wa bank akaipa bank au shirika lolote kiasi fulani cha pesa kwa ajili ya kuzizalisha kwa malipo maalum watakayokubaliana, hapa bank au hilo shirika linakua kama mzalishaji (investment manager). Banks za kiIslam zinatumia uwakala katika maeneo mengi kama vile Musharakah, Mudarabah, Salam,Istisnaa na Ijara.

Benks za kiIslam zinautumia uwakala ili kuzizalisha pesa za mteja kwa matumizi ya kila siku ya kibenk , uwakala unakua mkubwa kila mtaji wa mteja unapokua mkubwa.
Naomba pia ifahamike vizuri kua uwakala unakua kwa malipo maalum lakini pia unaweza kua bila malipo. katika makala hii tunazungumzia uwakala wenye malipo maalum. Kisheria Katika uwakala wenye malipo maalum muwakilishi (agent) anahaki ya kupokea malipo ya utangulizi mara tu baada ya kusaini mkataba wa kazi, lakini anaweza kuadhibiwa na hata kulipiswa faini pale tu itakapogundulika kua amevunja uaminif.
Ni vizuri tukakumbushan kwamba kuhitaji muwakilishi ni suala linajitokeza pale mtu anaposhindwa kutekeleza majukumu yake kwa sababu za kitaaluma, anapokua mbali na sehemu ya matukio au kwa sababu nyengine yoyote. Kazi kubwa ya muwakilishi ni kutoa huduma ipasavyo kwa masharti maalum ya yule anaemuwakilisha. Kwa upande mwengine unaposoma Quraan (43:32) utaona ya kwamba kuwakilishana ni mgawanyo wa kimajukumu kutoka kwa muumba mwenyewe ili maisha yaweze kuendelea, kwa upande mwingine ili binadamu washirikiane ktk nema. ‘It is We Who portion out [between them] their livelihood in this world [let alone the exalted rank of prophethood] and We raised some of them above others in ranks so that some may employ others in their work. But the Mercy of your Lord is better than what they amass’.

Uwakilishi katika banks zinazofuata sheria ya kiIalam inakua ni kazi ya kitaalam zaidi, kwa mfano, kazi ya kuuza, kununua, kukodi na kukodisha, kukopa na kukopesha, kushughulikia madeni, kufunga mikataba, kupokea malipo na kulipa ,kuongoza na kutetea haki za shirika kusafirisha pesa kutoka nchi kwenda nchi nyingine na kutoka mkoa kwenda mkoa mwengine na nyenginezo nyingi.

Muwakilishi wa Banks za kiIslam anaweza kua na jukumu zaidi ya moja, suala muhimu katika uwakishi ni kufahamika sifa za uwakilishi, kwa mfano, muda,malipo,kazi zenyewe na kadhalika. Kwa maana nyengine kama wakala ni wa kuuza au kununua inatakiwa iwe wazi anauza na kununua bidhaa gani?, ukubwa gani?, ubora gani? na mengine yote muhimu yanayohusu bidhaa .
Moja ktk tofauti kubwa zilizopo kati ya uwakala unaofuata sheria za kiIslam na ule ulazima wa kwamba shughuli anazowakilishwa mtendaji ni lazima ziwe halali ktk upande wa kisheria.
Kwa maelezo zaidi usisite kuwasiliana nasi. Tunatanguliza shukran.

Thursday 22 November 2012

Istisna'a

Mazingira yanayotuzunguka yana athari kubwa ktk shughuli zetu za kimaisha zikiwemo biashara. Kuna wakati ambapo misingi ya kawaida ya biashara halali inabidi itekelezwe kinyume na hali ya kawaida kwakua hilo litakua na wepesi kwa mmoja wa wanaofanya biashara.

Moja ktk biashara ambazo hazionekani kufuata misingi ya kawaida lakin ni halali na zimeruhusiwa ktk sharia ya kiIslam ni Istisna’a.
Istisna’a ni biashara ambayo inafanyika kabla ya vitu vinavyouzwa kutengenezwa. Ni lazima bei ya bidhaa ifahamike wakati wa makubaliano, kwa mfano, mnunuaji anatoa order ya kitu kitakachotengenezwa kama vile kabati, au nyumba ambayo itakabidhiwa baadae. Ili biashara ya Istisna’a iwe halali, bidhaa ambayo itatengenezwa ni lazima sifa zake ziwe wazi kwa kiasi ambacho haiwezi ikasababisha mzozo, kwa mfano ktk wakati wa leo kunaweza kua na catalogy ya vitu mbali mbali ambapo mteja anachagua kitu anachokihitaji.

Ni vyema tukakumbushana kwamba haiwezi kuitwa istasna’a kama bidhaa inayotaka kununuliwa tayari imeshatengenezwa na inajulikana, kama ambavyo Istisna’a haiwezi kufanyika ktk vitu ambavyo sio vya kutengeneza kama vile wanyama na matunda.
Hakuna ulazima wowote ktk biashara ya Istisna’a kwamba muuzaji awe ni yule mtengenezaji, kwani muuzaji anaweza kuingia mikataba maalum na mtengenezaji kwa ajili ya kutengeza vitu vinavyohitajiaka na nikwamisingi hiyo ambapo benki zinazofuata sharia za kiislam zinaweza zikaingia mkataba na watengenezaji wa bidhaa na zikauza kwa mteja kwa faida, kama ambavyo benki zinaweza kufanya kazi zote mbili ima kua muuzaji au mnunuzi wa bithaa ktk biashara ya Istisna’a. benki inaweza ikamuajiri mtu au shirika kama agenti wake kwa maridhiano ya pande mbili kwa ajili ya ufuatiliaji wa bidhaa na kuziuza pindi zitakapokua tayari au benki inaweza kumuwakilisha mtengenezaji wa bidhaa kama agenti wake. Moja ktk mambo ya kuzingatia ni kwamba mapatano endapo benki au mwingine yoyote ataitumia pande nyingine kama agenti wake, hizo zitakua ni biashara mbili tofauti, ya kwanza ni ile ya Istisna'a na yapili ni yauwakala. Benki inao uwezo vilevile wa kua na mshauri ambae atafuatilia mambo yanavyokwenda na kutoa ushauri kama bidhaa zinazotengenezwa zinafikia kiwango waliokubaliana. Gharama za mshauri huyo ni makubaliano kati ya pande mbili nani ambae atazitoa.

Istisana’a inaweza kutumika ktk biashara kubwa kama vile kujenga nyumba, madaraja, viwanda, barabara, bandari, viwanja vya ndege na mengineyo.

Kwakua biashara ya Istisna’a kuna wakati inachukua muda mrefu, bei waliopatana mteja na muuzaji inaweza ikabadilishwa kama hilo litafanyika kwa maridhianio kutoka ktk pande mbili. Unafuu mwingine ni ule unaohusiana na uwezekano wa mteja ktk biashara ya Istisna’a kulipa kidogodogo lakin ktk muda maalum watakao kubaliana. Kama hilo likifanyika basi mteja anaruhusiwa kisheria kuchukua rehani ya pesa anazozitoa kidogodogo

Ni vyema tukakumbushana kwamba ruhusa ya kulipa kidogodogo ktk biashara ya Istisna’a ni ruhusa ambayo imetolewa na wasomi wa zama tulizonazo na wametumia kitu kinachokulikana ktk sharia ya kiIslam kama (Istihsan) ambayo inajulikana kwa lugha ya kiingereza kama Juristi ‘prefence’ over strict analogy.
Kwa kawaida muuzaji anatakiwa anunue vifaa vyote kwa ajili ya bidhaa walioelewana, kama ikitokea kwamba mnunuzi amenunua vifaa na muuzaji ni mtengenezaji tu, muuzaji atachukua malipo ya bidhaa atakayoitengeneza lakin biashara hiyo haitazingatiwa kua ni Istisna’a.

Biashara ya Istisna’a haiwezi kuvunjwa na upande mmoja wakati kazi imeshaanza na kuna gharama ambazo zimeshatumika. Wasomi wengi wa wakati tulionao na Islamic fiqh Academy ya Organization of the Islamic conference (OIC) wanauzingatia mkataba wa Istisna’a kama mkataba ambao ni lazima utekelezwe (binding contract) kwa masharti fulani, kwa mfano kama bidhaa zimefikia kiwango na zimekabidhiwa ktk muda walioelewana mnunuzi hana hiyari ya kuleta masharti mengine yenye malengo ya kuvunja mkataba wake. Kama ikitokea mzaji au mnunuaji ameshindwa kutekeleza ahadi yake bila sababu za msingi, atatozwa fidia ambayo itatolewa kama msaada kwa wasiojiweza au utatolewa kwenye shughuli zozote za kheri na haitarhusiwa kutumiwa na upande wowote, kwani kufanya hivyo ni kinyume na sheria. Wanachoweza kupatana na ambacho sharia inaruhusu ni kupatana kwamba kwa mfano kama mteja atazitengeneza bidhaa kwa haraka kabla ya muda waliokubaliana basi ataipwa asilimia moja ziada au kama atachelewa atapunguziwa asiilimia moja malipo, hilo linawezekana na ziada hiyo haita takiwa kupelekwa ktk mashirika ya misaada.

Kwa hayo machache kuhusu biashara ya Istisna’a ni dhana yetu kwamba yatasaidia. Usisite kuwasiliana nasi kama kuna swali lolote kuhusiana na biashara hiyo.

Wednesday 29 August 2012

Salam (Non- participatory mode no 3)

Ktk mazingira ya kawaida kuna masharti yanatakiwa yakamilike ili biashara yoyote iwe halali kwa mujibu sheria ya kiislam, kwa mfano bidhaa zinazouzwa ni lazima ziwe zipo, kwa maana kama ni mazao basi yameshavunwa, sharti nyingine, muuzaji wa bidhaa ni lazima awe ni mmiliki halali wa bidhaa hizo. Biashara ya salam kidogo ni tofauti na biashara ya kawaida kwa maana kwamba ktk biashara ya Salam imeruhusiwa kisheria kuvunja baadhi ya masharti kama vile bidhaa kutokua tayari wakati wa mauziano.

Tunaweza tukajiuliza labda ni nini hasa Salam? Salam ni kulipa thamani ya bidhaa wakati bidhaa haijakua tayari na hilo linahusika sana na bidhaa za chakula na inajulikana kwa jina la kitaalamu kama ‘forward sale generally, for crops to be grown’.

Sababu hasa ya biashara kama hii ni kuwasaidia wakulima hasa wadogowadogo ili waweze kupata vitu wanavyovihitajia kama vile mbegu, mbolea, gharama za kutayarisha mashamba na kusaidia familia zao mpaka wakati wa mavuno. Hii imekuja kama badali ya kuwaepusha wakulima kuchukua mikopo yenye riba ambayo imekatazwa na ndio maana wameruhusiwa kuuza mazao yao kabla hayaja vunwa. Kwa lugha nyingine inaweza kusemwa kwamba hii ndio sababu ya msingi ya kuruhusiwa biashara kama hii.

Ni muhimu kutaja kwamba ktk jumla ya masharti muhimu ya Salam ni kujua tarehe ya kukabidhi bidhaa, taimu, aina na kiwango cha bidhaa. Kwa maana hiyo, biashara ya Salam inatakiwa ifanyike ktk vitu ambavyo vinaweza kupimika kwa vipimo maalum na kujulikana kiasi na kiwango chake, haya yote yanafanyika kwa ajili ya kuepesha ugomvi ambao unaweza kujitokeza baadae. Wanaofanya biashara ya Salam wana hiyari ya kupanga bei ya bidhaa wanavyotaka, lakin sana inakua ni bei ndogo kuliko bei ya soko. Mununuzi ni lazima atoe thamani kamili ya bidhaa kwa sababu asipofanya hivyo itakua ni kuuza deni kwa deni biashara ambayo imezuwiwa ktk sheria.

Kwa kawaida bidhaa za biashara ya Salam zinatakiwa kukabidhiwa kwa mnunuzi ktk wakati waliokubaliana, na kama ikitokea muuzaji ameshindwa kufanya hivyo bila sababu ya msingi, basi atapigwa faini na faini hiyo itapelekwa ktk mashirika ya misaada. Ispokua muuzaji wa bidhaa anaweza kuleta bidhaa kabla ya tarehe waliokubaliana kama hilo halitasababisha usumbufu kwa mnunuzi.

Benki zinazofuata sheria za kiIslam zinaweza kufaidika na bishara ya Salam lakin hazitaruhusiwa kupokea pesa kutoka kwa wateja wake, badala yake zitatakiwa zipokee bidhaa. Wakati huohuo benki hairuhusiwi kuuza bidhaa inazotegemea kuzipata ktk biashara ya Salam mpaka zitakapo kabidhiwa. Kwa upande mwingine, muuzaji wa Salam ambae sana ni benki anayo haki ya kudai dhamana au security kwa malipo ambayo ameyatoa na kama muuzajia akishindwa kufikisha bidhaa ktk wakati uliopangwa pasi na sababu ya msingi, basi mnunuzi anaruhusiwa kuchukua bidhaa kama zile sokoni kutokana na ile dhamana aliyoiweka muuzaji.

Wasomi wa kiIslam wameruhusu muuzaji na mnunuzi kupeana muda wa kufikiri (khiyr-al- shart) ambapo kila mmoja atakua na hiyari ya kuamua kwamba kweli anataka kuingia ktk mkataba. Kwa kuangalia hali halisi ya biashara ya Salam mnunuzi kwa kua anakosa nafasi ya kuona bidhaa anayotaka kuinunua (khiyar al-royat) atapewa nafasi nyingine inayojulikana kama (khiyar-al- aib) ikiwa na maana kwamba kama bidhaa alizoletewa ziko chini ya kiwango walichokubaliana, ana hiyari ya kuzikataa bidhaa hizo.

Ktk mazingira ya kawaida mnunuzi haruhusiwa kuuza bidhaa alizozinunua ktk biashara ya salam mpaka atakapo kabidhiwa bishaa ispokua anaweza kufanya kitu ambacho kinajulikana ktk sheria kama paralle salam ambapo mnunuzi anaweza kufanya mapatano ya kumuuzia bidhaa ya salam mtu mwingine wa tatu na sio Yule aliyefanya nae biashara mwanzo, kama ambavyo haitakiwa biashara hii ya pili iwe na mahusiano na biashara ile ya salam ya kwanza kwa hali yoyote. Kama yuleyule muuzaji wa kwanza atataka kununua tena bidhaa ileile aliyoiuza kwa salam, sheria haitamruhusu kufanya hivyo na kitendo hicho kitajulikana kama (a buy- back contract).

Kwa haya machache tutaishia hapa na kama kutakua na swali, maoni na ushauri wowote basi usisite kuwasiliana nasi. Shukran.

Thursday 23 August 2012

Ijarah (Non-participatory mode) no 2

Tukiendelea kuzungumzia mifumo isiyokua shirikishi, ktk makala hii tutazungumzia Ijara (kukodi).

Ijarah ni neno la kiarabu lenye maana ya kukodi (lease), ktk sheria ya kiIslam kukodi na kukodisha kunaruhusiwa kisheria ‘akasema mmoja wa wanawake, "ewe baba yangu muajiri. Kwa hakika, mbora wa ulie muajiri ni mwenye nguvu muaminifu" (Quraan: 28:26 ).

kukodi kunatumiwa katika maana mbili tofauti, maana ya kwanza ni kukodi huduma kutoka kwa mtu, watu au shirika fulani kwa malipo maalum mliyopatana, na hapa ndipo tunapata muajiri na muajiriwa kama ifuatavyo, Yule anaetoa huduma anaitwa muajiriwa na Yule anaepata huduma anaitwa muajiri. Kwa mfano kama A anampa kazi B kama meneja mauzo kwa malipo maalum (lessor) kila mwezi,wiki,au mwaka, basi A anakua muajiri na B anakua muajiriwa. Kutokana na mfano huo tunajifunza ya kwamba unaweza kumuajiri mwalimu,mwanasheria,Daktari nakadhika. Pia mtu anaweza kua muajiri mahali fulani na muajiriwa mahala kwengineko na kuendelea.

Maana nyingine ya kukodi ni pale mtu, watu, kikundi, au shirika fulani wanapokodi kitu fulani kutoka kwa mtu, watu au shirika fulani na si kumkodi mtu mwenyewe, kwa mfano A kukodi nyumba ya B, au shamba ,gari ,tractor kwa muda maalum na kwa malipo maalum yanayoitwa kodi (lessor). Hapa tuweke wazi kidogo kua katika lugha ya Kiswahili malipo anayopewa mfanyakazi kwa huduma aliyoitoa yanaitwa mshahara kwa kua mara nyingi hutolewa kila mwezi, mwezi kwa kiarabu huitwa (shahri), na ndio maana kile kilichotolewa kila mwezi kikaitwa mshahara.

Aina hizi mbili za Ijarah (lease) zimezungumziwa na uIslam, na kila moja ina sheria zake maalum, lakini hii ya pili ndio inayotumika sana na benki zinazofuata sheria za kiIslam, na katika uwanja wa biashara na uekezaji kwa ujumla, na aina hii ya kukodisha ndio ambayo itazungumziwa kwa kirefu zaidi.

Sheria muhimu za kukodi (leasing)
1- Kukodi kuwe ni makubaliano au mikataba ambayo mmiliki wa kitu anahamisha matumizi ya kitu hicho kwa mtu mwengine kwa muda maalum na kwa malipo maalum.

2- Kitu kinachokodiswa kiwe na thamani ya matumizi,kwa maana hiyo vitu visivyo nathamani kimatumizi havikodiswi. Unaweza kukodisha gari,nyumba n.k.

3- Kitu kinachokodiswa kinabaki ni mali ya mmiliki ,na matumizi tu yatamilikiwa na mkodishaji. Vitu ambavyo havibakii na hutoweka vinapotumiwa kama mafuta, vinywaji, vyakula na kadhalika havikodishwi kisheria.

4- Katika mali inayokodiswa kama kutatokea uharibifu unaotokana na mkodishaji , basi atalipa na kama unamuhusu mmiliki basi atalipa mmiliki mwenyewe. Kwa mfano kodi za jengo zinazolipwa serikalini atalipa mwenye jengo na kodi za biashara zinazolipwa(TRA) atalipa mkodishaji.(isipokua kama kutakua na makubaliano maalum).

5- Muda wa kukodi ujulikane mwanzo na mwisho kabla ya kutumia mali iliyokodishwa.

6- Mali iliyokodishwa itumike kwa madhumuni yale tu yaliyoainishwa katika mkataba. Kama hayakuainishwa basi yawe katika matumizi ya kawaida na afahamishwe mmiliki matumizi hayo kabla.

7- Kama kutatokea uharibifu wowote wa kimakusudi katika mali iliyokodishwa basi mkodishaji atatakiwa kulipa alichoharibu.

8- Mali iliyokodiswa inakua katika hatari (risk) ya mmiliki katika kipindi chote cha ukodishwaji kwa maana uharibifu wowote utakaotokea nje ya uwezo wa mkodishaji utakua nijukumu la mmiliki.

9- Mali inayomilikiwa na wamiliki zaidi ya mmoja pia inaweza kukodiswa, mkodishaji atalipa kiasi cha kodi inayotakiwa kama kodi moja na kisha kodi itagawanwa kwa kiasi cha asilimia za wamiliki.

10- Mali inayomilikiwa na mtu zaidi ya mmoja haitakodiswa na mtu mmoja mmoja , isipokua kama kila mmoja anamiliki sehemu yake maalum, atakodisha sehemu yake tu.

11- Ni muhimu sana katika ukodishaji unaokubalika uwe unafahamika kwa njia ya uwazi kabisa kwa wahusika wote, kwa mfano kama A anamwambia B nakukodisha moja ya maduka yangu mawili, B akasema nimekubali, kukodi huku si sahihi mpaka aainishe duka gani kati ya hayo mawili analomkodisha?

Baadhi ya tofauti zilizopo kati ya kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam na kule kusikofuata sheria za kiIslam

Ktk kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam gharama za kukodisha zinaanza wakati bidhaa iliyokodishwa itakapofika kwa mteja, wakati ktk kukodisha kusikofuata sheria za kiIslam, gharama za kukodisha zinaanza haraka mkodishwaji atakapolipa gharama hata kabla ya kufikishiwa alichokikodisha.

Ktk kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam hatari zote zinazohusiana na bidhaa zitabebwa na benki iwapo mkodishwaji hatasababisha madhara yoyote kwa makusudi au uzembe, wakati kukodisha kusikofuata sheria za kiislam hatari zote zinazohusiana na bidhaa zinabebwa na mteja bila kujali mazingira yaliyosababisha.

Kwa maelezo zaidi Fuatilia makala ijayo

Wednesday 22 August 2012

Murabaha (Non- participatory mode) no 1

Wasomi na wachumi wa kiIslam wanapendelea benki za kiIslam zitoe huduma kwa kutumia mifumo shirikishi ambayo ktk moja ya sifa zake kuu ni mteja kushirikiana na benki ktk faida na hasara. Ingawaje, kiufundi mifumo inayotumika sana ni ile mifumo isiyokua shirikishi (non-participatory modes), ikiwemo murabaha, Ijara na salam, ktk makala hii tutazungumzia murabaha.

Murabaha ni aina ya biashara ambayo inakubalika ktk sheria ya kiIslam ambapo muuzaji anamtajia mnunuzi thamani aliyonunulia bidhaa na anaongeza faida yake ambapo sana, mnunuzi atalipa thamani ya bidhaa hiyo pamoja na faida waliyokubaliana kidogodogo na kwa muda unaojulikana.

Bank za kiIslam zinatumia murabaha pale benki inaponunua bidhaa fulani kulingana na matakwa ya mteja na ikamuuzia mteja bidhaa hiyo kwa thamani iliyonunulia na kuongeza kiasi cha faida. Kimsingi, mteja anailipa benki kidogodogo ktk muda watakaokubalina kwa sababu kama angekua na uwezo wa kulipa kwa pamoja asingekua na haja ya kununua bidhaa hiyo kwa kutumia benki, ingawaje, kisheria hazuwiliwi kufanya hivyo. Kiwango walichokubaliana hakitakiwi kubadilika, vinginevyo mazingira ya riba yanaweza yakajengeka.

Baadhi ya masharti ya murabaha:

1- Muuzaji wa bidhaa ni lazima awe ni mtu anaeruhusiwa kuuza kisheria, kwa mfano, huwezi kufanya biashara na mtoto mdogo.

2- Muuzaji ni lazima amiliki kisheria kile anachokiuza

3- Kinachouzwa ni lazima kijulikane

4- Bei ya kitu ni lazima iwe maalum na isibadilike, kwa mfano A ametaja shilingi 500 kua ndio bei ya bidhaa fulani atakayo muuzia B kwa muda wa mwezi mmoja, lakin kama ikipita miezi miwili A atamtaka B alipe Shilingi 510. Ktk hali kama hii bei ya bidhaa itakua haina uhakika, na mauziano ya namna hiyo yatakua ni batili.
Na kuna masharti mengine ya murabaha ambayo yatawekwa wazi zaidi ktk makala zinazokuja.

Uhalali wa kupanga bei maalum na muda maalum na maswali yanayoweza kujitokeza.

Wasomi wengi ktk wakati tulionao wanahalalisha kuuza bidhaa kwa bei tofauti ktk kipindi tofauti na wanaliona hilo ni kama mabadiliko ya kiuhalisia yanayotokana na mahitaji ya soko (supply and demand),kwa mfano bidhaa inaweza kuuzwa sokoni kwa Sh 500 leo na bidhaa ileile ikauzwa kwa Sh 510 kesho au ikawa inauzwa kwa bei tofauti wakati uleule ktk soko jingine. Kwahiyo ni halali kwa muuzaji kumuambia mteja kwamba kama utanunua bidhaa hii leo nitakuuzia kwa Sh 500 lakin kesho itauzwa kwa Sh 510. Mabadiliko hayo ya bei yanatakiwa yatokane na hali halisi ya soko na yasionekane kama ni fidia ya wakati. Ktk mazingira kama hayo muuzaji haruhusiwi kutumia hadaa kwa ajili ya kupata bei nzuri.

Tofauti ya murabaha ktk benki za kiIslam na zile zisizokua za kiIslam
Ni vyema tukakumbushana kwamba murabaha inatumiwa sana na benki za kiislam na zisizokua za kiIslam ktk biashara mbalimbali, kwa mfano murabaha unaweza kutumika kwenye viwanda vya muda mfupi, ktk biashara ya nyumba na kununulia mashine za kufanyia kazi. Wakati murabaha hauhusiani na banki za kiIslamu tu, kuna tofauti ya msingi kati ya benki hizo mbili, kwa mfano faida inayopatikana ktk benki za kiIslam haihusiani na kitu kinachojulikana kama (opportunity cost of money).

Tofauti nyingine ni ile inayohusiana na mteja kushindwa kulipa kwa kipindi walichokubaliana na benki. Kwa benki za kiIslam, itategemea kwanini mteja ameshindwa kulipa kwa taimu aliyopangiwa, kwa mfano kama kuna sababu za msingi basi ataongezewa muda, na kama hana sababu za msingi basi anaweza kupigwa faini lakin faini ile haitatumiwa na benki ktk shughuli zake na badala yake itatolewa bure kwa mashirika ya misaada. Maswala haya yatazungumziwa kwa ufafanuzi zaidi baadae.

Kwa kuzingatia mazingira ya kibiashara ktk wakati tulionao, murabaha unahusiana na mikataba mbalimbali kama vile maombi ya mteja kununua bidhaa Fulani, ahadi ya mteja kwamba atainunua hiyo bidhaa, ahadi ya wakala na mkataba wa kuwepo maombi na kukubali kutoka pande zote mbili benki na mteja. Ahadi ya kununua bidhaa kwa mteja kutoka benki ni lazima itekelezwe (binding), kwa maana mteja anatakiwa kisheria atekeleze ahadi yake na kama akivunja ahadi yake baada ya benki kununua bidhaa waliokubaliana, mahakama inaweza kutumika kumlazimisha mteja kutekeleza ahadi yake. Hilo linaweza kufanyika kwa kutumia njia mbili, ima mteja kununua kitu alichoahidi au kulipa gharama zilizotumika ktk swala hilo, lakini hilo la mteja kupigwa faini, halizingatiwi kama ni badali ya (opportunity cost) kwani kufanya hivyo kutajenga mazingira ya riba. Pamoja na mambo mengine benki ili iwe na uhakika na inachokifanya inaruhusiwa kisheria kumlazimisha mteja kununua kitu kinachojulikana kama Hamish jiddiah ambayo ni kiasi fulani cha pesa kitakachotolewa kama deposit ambayo itafahamisha kwamba kweli mteja ana nia ya dhati ya kununua bidhaa kama alivyoahidi

Sheria inasemaje kama mteja akilipa mapema kuliko muda aliopangiwa?

Kwa kawaida kiwango cha faida kilichowekwa ktk murabaha hakibadiliki kwa mteja kulipa mapema, ispokua benki inaweza kuhamasisha wateja wake kulipa mapema na kwahivyo basi wakaahidi wateja wao aina fulani ya zawadi. Ktk mazingira ya kawaida wasomi wa kiislam (scholars) hawaruhusu mtu kulipa mapema kwenye murabaha kwani itakua haina tofauti sana na biashara ya riba ambayo imekatazwa. Accounting and Auditing Organization for Islamic financial Institutions (AAOIFI’s) wanaona kwamba, kama benki haikumuahidi mteja kitu chochote kwa kulipa deni lake haraka, basi benki itakua na hiyari kati ya kutoa zawadi na kukataa. Hayo yalikua ni maelezo ya murabaha kwa mukhtasar. Kwa haya machache tutaishia hapa na kama kutakua na swali lolote basi usisite kuwasiliana nasi. Shukran

Saturday 2 June 2012

mfumo shirikishi (participatory mode) no 2

Mudarabah

Baada ya kuelezea musharakah ambao ilikua ni mmoja kati ya mifumo shirikishi (participatory modes), ktk makala hii tutaelezea aina nyingine ya mfumo shirikishi ambayo ni mudarabah (co-partnership) na mfumo huu unatumiwa sana na bank za kiIslam kutokana na faida nyingi zilizopo katika mfumo huu. Wachunguzi wa mambo ya kibiashara wanadai kwamba mataifa na mashirika mbali mbali, na hata watu binafsi duniani wanafaidika sana na mfumo huu, kwa mfano nchi kama Tanzania kwa kushirikiana na bank za kiIslam inaweza ikautumia mfumo huu katika kilimo kwanza badala ya mfumo uliopo sasa kukopesha(loarn). Kwa kuliweka wazi zaidi hilo tumeona ni muhimu tuanzie kwa kumfahamisha msomaji nini maaana ya mudarabah (co-partnership).


Maana ya mudarabah (co-partnerhip)

Mudarabah ni aina maalum ya ushirika (co-partnership) kati ya watu wawili na zaidi au makundi mawili na zaidi, upande mmoja unatoa mtaji (capital) upande huu unaitwa rabbu-ul-maal (investor or financier), na upande mwengine unatoa juhudi ktk kusimamia mtaji huo na unaitwa mjasirimali(mudarib -entrepreneur- or- labour). Kwa mfano Bank itakapotoa million 20,000,000 ikampa Ahmadi kuzizalisha, katika mfano huu bank itaitwa (investor) na Ahmadi ataitwa mjasirimali (interprenuer or labour).


Kwa kawaida ktk mudarabah inakadiriwa kua mjasirimali ni mshirika ktk biashara lakini hakutoa mtaji wa aina yoyote zaidi ya juhudi, kwani akitoa mtaji biashara hiyo kitaalamu itajulikana kama musharakah ambayo imeelezewa ktk makala iliyotangulia na sio mudarabah ambayo tunailezea hapa. Kutokaana na maelezo hayo hapo juu tunaona kwamba mudarabah ni kushirikiana katika faida kati ya mtaji(capital) na uzalishaji(labour).


Ili kuongeza uzalishaji katika jamii na ufanisi katika kazi uIslam unaruhusu kwa rabbul-mal (provider or investor) kufanya biashara hiyo hiyo na watu zaidi ya mmoja, kwa mfano bank inaweza kumpa mtaji Salim na Ahmad wote wakafanya biashara hiyo hiyo kwa pamoja na watagawawana faida kulingana na makubaliano yao. Ktk sura kama hii uhusiano kati ya Ahmad na Salim utajulikana kama musharakah wakati uhusiano kati yao wote wawili na bank utajulikana kama mudarabah.


Mudarabah ni ushirika ambao unatumika sana katika nchi zilizoendelea na hasa nchi za Ulaya magharibi na USA, kwa mfano katika maduka makubwa kama Tesco, Asda na mengineyo, wamiliki wa maduka haya wanafanya murabaha na mameneja wakubwa wa maduka haya. Ingawaje, biashara zao wakati mwengine hazitimizi baadhi ya masharti ya mudarabah kama swala zima linalohusiana na hasara kama ikitokea.


Ni ukweli usiopingika kua mudarabaha ni ushirika ambao unawafaidisha wenye mali na wale wenye elimu na vipaji mbali mbali, na ushirika aina hii kwa kiasi kikubwa umekua ni sababu ya maendeleo katika nchi nyingi za kimagharibi.


Aina za mudarabah

Mudarabah unagawanyika katika sehemu kuu mbili


1-Kuna Mudarabah usionamasharti (unrestricted- mudarabah) maana yake ni pale washirika na hasa mwenye capital (investor, finencier) asipoweka masharti yoyote katika ushirika wao.


2- mudarabah wenye masharti (restricted-mudarabah) ni ule ambao rabbul-ul-mal (investor)atakapoweka masharti maalum ndani ya biashara, masharti haya yanaweza yakawa katika aina ya biashara, mahali pa biashara na kadhalika, katika ushirika wa aina hii mtoa mtaji (investor) hatakua na haki yoyote ya kudai msingi wake kama itatokea hasara yoyote isipokua tu kama mjasirimali (interprenue-labour) atakwenda kinyume na misingi ya ushirika wao.


Ni vizuri kukumbusha kua kisheria mjasirimali anayo haki ya kufanya kitu ambacho kitaleta faida zaidi ndani ya ushirika wao ingawa atatakiwa amfahamishe mtoa mtaji (investor) juu ya alichokibuni ili kujilinda kama itatokea hasara yoyote. Kama hatamfahamisha mtoa mtaji naikatokea hasara yoyote atatakiwa alipe hata kama alikua na nia njema katika biashara yao.


Mgawano wa faida

Ili mudarabah uwe sahihi ni lazima washirika waweke wazi tangia mwanzo mgawano mzima wa faida itakayopatikana kwa kiwango cha asilimia. Mambo muhimu yatakayo angaliwa katika kujadili faida nipamojana kiasi cha faida, muda wa kugawana na ,mahali, kwa mfano washirika wanaweza kukubaliana kugawa faida kila mwaka, mwezi, au kila watakaponunua na kuuza na kadhalika. Hakuna hasa masharti maalum yaliyowekwa na sharia katika ushirika cha msingi tu nikuwa masharti yasiwe kinyume na sharia, maana yake nikua masharti ya ushirika yataachiwa washirika wenyewe, kwa mfano washirika wanaweza kugawana faida sawa kwa sawa au wanaweza wakagawa tofauti, pia washirika wanaweza kukubaliana kugawana sehemu tu ya faida na nyengine ibaki waje kugawa baadae.


Ni vizuri kujua pia kua mgawano wa faida unaweza kubadilika kulingana na biashara, kwa mfano endapo watakua wanashirikiana ktk biashara zaidi ya moja, mtoa mtaji anayohaki ya kusema kua katika biashara ya madini awe na 50% ya faida, lakini katika biashara ya magari awe na 60%, pia anayohaki ya kusema kua kama utafanya biashara nje ya nchi nitataka 60% ya faida na kama unafanya ndani ya nchi nitataka 40%. Mifano hii nikutaka kumfahamisha msomaji kwamba sharia ya kiislam imewacha masharti ya ushirika yatoke kutoka katika pande zinazoshirikiana muhimu tu yasiwe ni kinyume na sharia.

Ni muhimu pia tukakumbushana kwamba kwakua ktk mudarabah kuna mgawano wa faida, basi hakuna mshahara wowote atakaostahiki mjasirimali (labour) na hii wamekubaliana madhehebu zote (Islamic schools of thought). Kuhusu gharama zinazojitokeza katikati ya uzalishaji kama vile matumizi ya kila siku ya mjasirimali, wanachuoni wengi wanaona kua gharama zitokane na mtaji wa biashara yenyewe ingawaje Imam Ahmadi amedai kua zitatoka mfukoni mwa investor lakini Abuu Hanifa anadai kua gharama zitatoka kwa mjasirimali isipokua kama atafanya biashara nje ya mji wake hapo ndio atadai gharama muhimu kama za chakula, makazi nakadhalika. Ikitokea mjasirimali ametumia gharama zake binafsi, basi zitatolewa na kurudishiwa kabla ya mgawano wa faida.


Kuvunja au kumalizika mudarbah

Mudarabah unaweza kuvujwa wakati wowote ilimradi washirika au mmoja kati ya washirika wapeane taarifa. Kama kutakua na faida yoyote wakati wa kuvunja mudarabah basi watagawana kama walivyokubaliana, na kama hakuna basi mtoa mtaji(investor) atachukua alichotoa na hapo mudarabah utakua umefika mwisho. Inaweza ikatokea kua bishara inayofanyika sio fedha taslim ni kitu kama mashine,magari nakadhalika hapo mali hizo zitauzwa kwanza ndipo washiriki watagawa kilichopatikana, kwa mfano kama mtoa mtaji ametoa kiwanda cha sabuni kiwanda hicho kinabaki kua ni mali yake na sabuni zilizopo zitauzwa ndipo wagawane faida kwa kiwango walivyokubalian.


Kama washirika wamekubaliana muda maalum wa ushirikiano wao basi muda ukifika ushirika utakua umemalizika hapo, Kwa mfano walikubaliana ushirika wao uwe wa miaka miwili basi baada ya miaka miwili ushirika utakua umemalizika bila kuhitaji maelezo yoyote, hilo linakubalika katika Madhabu(Islamic schools of thought) ya Hanbali na Hanafi ingawa limepingwa na Shafi na Maliki. Madai ya kupinga kwao ni kwamba hili litawanyima washirika uhuru kama wanataka kuvunja ushirika na hili linaweza kusababisha uzito fulani kwa washirika.


Ingawaje, inaonyesha kua kumpa mshirika uwezo wa kuvunja ushirika wakati wowote hili nalo kwa wakati tulionao ambao bishara nyingi ni za viwanda ambazo zinahitaji muda kuzizalisha litasababisha matatizo pia. Kwa mantiki hiyo, itakua ni vigumu kumpa mshirika nguvu zisizo na mipaka katika kuvunja ushirika na imependelewa kua washiriki wasubiri mpaka uzalishaji ukamilike hata kama wamewekeana muda maalumu na umeshakamilika, isipokua zikitokea hali zisizokua za kawaida ambazo ni za kuvunja sharia.


Baada ya muda waliopatana washirika kukamilika na ikatokea kua bado washirika hawa wanataka kushirikiana, basi watafunga mikataba mipya. Kwa njia nyingine ni kwamba ushirika unakwisha kwa kufa mmoja wa washirika ispokua kama wanaomrithi watapenda kuendelea na ushirika hapa yatahitajika makubaliano mapya pia. Inaweza ikajitokeza kua mfu amezikwa kutokana na mali zake au ana deni au ameusia kitu kifanyike kutoka katika mali zake kiasi hicho kitatolewa katika fungu lake na kitakachobakia kitaendele kua katika ushirika.


Ikumbukwe kwamba mtume (sws) alishirikiana na wasio waislam katika kununua, kukopa na katika mambo mengine yaliyo ruhusiwa kiislam, na hivyo hivyo waislam wanaweza kushirikiana na wasio waislam katika mambo ikiwemo biashara zilizoruhusiwa kiislam.


Ukweli ni kwamba mwenye akili ya kawaida tu hatosita kukubaliana na mfumo huu wa ushirika kutokana na faida zilizopo. Miongoni mwa faida zake ni kuunganisha vipaji mbali mbali kufanya kazi pamoja, kwa mfano mtu anaweza kumiliki mali lakini akashidwa kuzisimamia mali hizo kwasababu moja au nyengine kama vile ugonjwa, kukosa elimu, au mtoto mdogo alieachiwa mali na wazazi wake waliofariki na kadhalika, au mtu anaweza kua na ujuzi fulani labda uashi,kulima nakadhalika lakini akawa hana vyanzo vya kuanzia kazi, ili kuifanya jamii iweze kufaidika kila mmoja na mwenzie uislam uliliona hilo ndipo iliporuhusiwa kuchanganya vipaji kwa manufaa ya jamii nzima Quraan (38:24).


Kwa kumalizia tu tunakumbushana kwamba kwa sababu mudarabah ni mapatano kati ya washirika wawili ni lazima masharti ya mkataba (contract) yakamilike na mapatano yenyewe yawe ktk mambo ambayo yanaruhusiwa kisheria. Kama kutakua na kitu chochote ambacho hakiko wazi kuhusu mtaji au asilimia ya faida watakayogawana basi mudarabah utakua ni batili.






Tuesday 8 May 2012

Mfumo shirikishi (Participatory mode) no 1

Ktk makala iliyopita tulizungumzia mifumo ya uchumi wa kiIslam kua ni mfumo shirikishi (participatory), mfumo usiokua shirikishi (non- participatory) na mfumo upitishaji (Accessory). Vilevile tulieleza kwamba mfumo shirikishi unahusika na sehemu mbili ktk biashara ambazo ni mudarabaha na musharaka (partnership), ktk makala hii tutaelezea musharaka kwa ufafanuzi zaidi.

Ushirika (partnership)

Sheria ya kiIslam imejaa aina mbalimbali za biashara, uwekezaji na mengineyo ambayo yanaweza yakamuingizia mtu faida ktk mtaji wake au ujuzi alionao. Moja ktk biashara na ambazo zilijulikana mapema kabisa ktk uIslam, ni kitu kinachojulikana kama (shirkah) ambayo kwa lugha ya kibiashara ktk wakati tulionao inajulikana kama ushirika (partnership).

Ushirika maana yake ni pale watu wawili au zaidi ya wawili watakaposhirikiana ktk biashara halali kwa kuchanganya mitaji yao (capital), juhudi au ujuzi (labour) au gharama (credit worthness) na wakawa na haki na majukumu ktk ushirikiano huo. Wakifanya hivyo watashirikiana faida au maslahi yaliyopo ktk biashara hiyo kulingana na mapatano yao kama ambavyo watashirikiana hasara kulingana na kiasi cha kila mmoja alivyoshirika ktk mtaji. Ni muhimu kukumbushana kwamba faida ya washirika inaweza kukadiriwa kwa asilimia kama vile 30% lakin faida yenyewe haiwezi kujulikana ni kiasi gani mpaka itakapopatikana. Moja ktk vitu muhimu vya kukumbushana ni kwamba ni lazima makubaliano ya kugawana faida yafanyike mwanzo kabla ya kufanyika chochote na kusiwe na uhakika (guarantee) wa kiwango cha faida (rate of return), vinginevyo ushirikiano huo utakua ni batili. Kiwango hicho cha faida kinaweza kubadilishwa wakati wowote kabla ya faida kupatikana lakin hilo haliwezi kufanyika kama faida tayari imeshaingia.

Kuna aina nyingi za ushirika ktk sheria ya kiIslam kulingana na tofauti zilizopo za kimadh habu (Islamic schools of thought) kama vile madh habu ya imam Shafii, Malik, Hanbal na Abuu Hanifa. Ingawaje swala la madh habu na athari zake ktk bank za kiIslam litajadiliwa baadae.

Aina za ushirika

Sheria ya kiIslam imeliangalia swala la kushirikiana ktk sura kuu mbili. Sura ya kwanza inajulikana kama ushirika ambao sio kwa ajili ya biashara (shirkah-al-milk) na sura ya pili ni ile ya kushirikiana kwa mikataba maalum (shirkah-al- aqd).

Moja ktk tabia za kushirikiana ni kwamba, kuna wakati watu wanaweza kushirikiana hata bila ya hiyari yao kama vile kuachiwa nyumba ya urithi. Makala yetu italiangalia kushirikiana kule kwa hiyari na kwa mikataba maalum.

Kushirikiana kwa hiyari na kwa mikataba maalum kunagawanyika ktk sehemu kuu mbili mudarabah na musharakah. Lakin kwa kua tunazungumzia musharakah (partnership) basi hapa tutaungalia musharaka tu.

Kuna aina karibu tatu za kushirikiana kwa mikataba maalum ambazo watu au kikundi cha watu au taasisi mbalimbali zinaweza kushirikiana.

1- kushirikiana ktk mtaji na juhudi (shirkah-al-amwal).
2- Kushirikiana ktk kazi na huduma lakin sio mtaji (sharikah-al-amal).
3- Kushirika ktk nia njema na gharama (credit worth) lakin hakuna mtaji unaotumika. hiyo inajulikana kama (shirkah-al-wujuh).

Kwa ujumla, wanaoshirikiana wanakua na haki sawa lakini sio lazima wawe na majukumu sawa. Musharakah ktk uislam unafanana sana na uschumi wa sasa hivi na kitu kinachojulikana kama (limited partnership structures and the holding for voting shares in a limited company).
Kwa kawaida wanaoshirikiana watakapotoa mitaji yao kuiingiza kwenye biashara, mali zao zote (assets) zitakua zinamilikiwa kwa pamoja kwa kiwango cha kila mmoja alivyoshiriki ktk mtaji.

Kushirikiana kwa ajili ya uwekezaji kunaweza kugawanyika kwenye sehemu kuu mbili

1- Kushirikiana kwa kudumu (permanent musharakah)
2- Kushikiana ambako sio kwa kudumu (diminishing musharakah)

Kushirikiana ambako sio kwa kudumu ni kule ambako mmoja wa washirika anaamua kuchukua kiasi cha ziada kila faida inapopatikana kwa malengo ya kutaka kutoka baadae ktk ushirika, atakapotimiza kiwango walichokubaliana basi anakua ametoka ktk ushirika na mali yote iliyobakia inakua ni ya upande uliobaki. Hii itaelezewa kwa ufasaha zaidi baadae.

Jinsi banki za kiIslam zinavyofanya musharakah

Tuchukue mfano wa musharakah ambao sio wa kudumu (diminishing musharakah). Mteja inaifuata bank kwa ajili ya kufanya ushirika wa kununua nyumba lakin mteja ana asilimia 20 tu ya thamani ya nyumba, kwahiyo bank inatoa asilimia 80 na baada ya nyumba kununuliwa inakodishwa kulingana na bei ya soko. Mteja analipa asilimia 80 ya kodi kwakua tayari ameshalipa asilimia 20 na analipa kiasi kingine cha kupunguza thamani iliyonunuliwa nyumba. Mwisho wa muda waliokubaliana kwa mfano miaka kumi, nyumba inakua ni mali ya mteja. Baada ya kumalizika muda uiokadiriwa bank itakua imerudisha pesa yake na imefaidika na kodi iliyotolewa ktk kipindi hicho. Hayo yote ni mbali na gharama nyingine zitakazotolewa na bank kama vile bima na kodi nyingine kama VAT.

Moja ktk vitu muhimu vya kukumbushana ni pamoja na kwamba kuna maoni tofauti ya madh habu (Islamic schools of thought) kuhusiana na swala zima la kugawana faida na hasara kwa wale wanaoshirikiana. Imam Malik na Shafii wanaona kwamba ili kushirikiana kuwe sahihi ni lazima kila mshirika apate faida kulingana na alivyoshiriki ktk mtaji, wakati imam Ahmad anaona kwamba faida inaweza kutofautina na kiwango akichoshiriki mtu ktk mtaji kama walioshirikiana wakiamua hivyo bila ya kulazimishwa tangia mwanzo. Imam Abu Hanifa anachukua msimamo wa kati ktk rai hizo mbili kwa kusema, kiasi cha faida kinaweza kutofautina na kile cha mtaji ktk mazingira ya kawaida, ingawaje, kama mshiriki mmoja aliweka masharti ya kwamba hatashiriki kwa kitu chochote baada ya kutoa mtaji (sleeping partner) basi kiwango chake cha faida hakiwezi kua zaidi ya kiwango cha mtaji aliotoa.

Kitu kingine muhimu cha kukumbushana ni kwamba kwa sababu ushirika ni uhusiano kati ya pande mbili tofauti ni lazima masharti yote ya kufunga mikataba yakamilike. Kwa mfano pande zinazoshiriki ktk mikataba ni lazima zinaruhusiwa kisheria kufunga mikataba, kwa mfano huwezi kufunga mkataba na mwendawazimu. Vilevile kusiwe na aina yoyote kulazimishana, kutumia udanganyifu na mengineyo. Kuna swala linalohusiana na mteja kushindwa kulipa kiwango alichopangiwa kwa sababu zozote, hayo yataadiliwa ktk makala zinazokuja.

Wasiwasi wa mteja au bank kupata hasara ktk ushirika

Kuna wasiwasi uliojitokeza kwamba ushirika una uwezekano mkubwa wa kuleta hasara kwa bank za kiIslam, hasara ambayo itawakumba hata wale walioshirikiana na bank wakiwemo wateja na hilo litawafanya wateja kuikimbia kuweka pesa zao bank kwa ajili ya uwekezaji.
Hoja hiyo imepanguliwa kama ifuatavyo. Uhakika ni kwamba kabla ya bank kufanya biashara yoyote inafanya uchunguzi kwanza kwamba biashara hiyo ina uwezo kiasi gani wa kuingiza faida (Feasibility study) na hata ktk bank zisizokua za kiIslam wanafanya hivyo kwanza na wakihisi kua biashara hii inaweza isiingize faida, wanakataa kujihusisha na biashara hiyo. Pamoja na mambo mengine bank haifanyi biashara ya ushirika peke yake, inafanya biashara nyingi kitu ambacho sirahisi kupata hasara ktk biashara zote hizo. Moja ktk maoni ni kwamba ushirika kama utafanywa ipasavyo, na hatua muhimu za kudhibiti hasara zitachukuliwa, mategemeo ya kuingiza faida ni makubwa zaidi kuliko yale yaliyopo ktk bank za riba.

Pamoja na kusema hivyo, uchumi wa kiIslam ni lazima ujiridhishe kwamba faida yoyote itakayoingia ni lazima iambatane na baadhi ya hatari (risk), hatari hiyo inaweza kupunguzwa kwa kutumia wataalam au kwa kufanya biashara tofauti tofauti ambapo moja ikipata hasara nyingine inapata faida. Lakin ni lazima tukubali kua hakuna uwezekano wa kuhakikisha kua biashara fulani haiwezi kupata hasara kabisa. kama unataka faida ni lazima ukubali uwezekano wa kupata hasara. Kama watu wakiwa na fikra hizo basi uwezekano wa kutokea tatizo kama ikipatikana hasara ni mdogo sana. Moja kati ya matatizo ya watu kutaka faida tu bila kukubali hasara ni tatizo linalotokana na mfumo wa kuitenganisha bank na uchumi wa kawaida na kudhania kua ni vitu viwili tofauti na kwamba bank haina uhusiano wowote na hasara inayotokana na biashara, hilo limepelekea baadhi ya bank kumuahidi mteja kiwango maalum cha faida bila kujua biashara itakwendaje kitu ambacho kimeshiriki kwa kiasi kikubwa ktk matatizo ya uchumi yanayoukumba ulimwengu.
.
Kuvunja ushirika

Kwa kawaida kuvunja ushirika kunaweza kutokea iwapo walioshirikiana walipatana hivyo tangu mwanzo wa ushirika, aidha inawezekana kuvunja ushirika kama moja kati ya sababu zifuatazo itatokea.

1-Anaetaka kujitoa ktk ushirika atakapotoa taarifa ktk kipindi cha mwisho wa musharakah ktk kipindi ambacho mali zote ziko ktk mfumo wa fedha taslim (cash). Kama kutakua na asset ambazo hazipo ktk mfumo wa cash itabidi zitiwe thamani ya cash vininevyo wahusika wengine wa ushirika wanaweza kugawana asset hizo na ikiwa ni vitu ambavyo haviwezi kugawanyika kama vile mashine basi itabidi ziuzwe.

2- Kama mmoja wa washirika akifariki basi ni juu ya warithi kuendelea na ushirika au kujitoa ambapo watastahiki fungu lao kwa utaratibu tuliyoutaja juu.
3- Kama ikitokea mmoja wa washiriki hana uwezo wa kuendelea na ushirika kwa tatizo lolote kama vile ugonjwa na mengineyo.

References

Mughni Libn Qudamah (mlango wa sharikah) Vol no 14.

Rahman, H. (2005), Financing banking through musharaka principles and applicalication. Adelaide: University of Adelaide.

Usman, T. “PRINCIPLES OF SHARI’AH GOVERNING ISLAMIC INVESTMENT FUNDS” Available from http://www.kantakji.com/fiqh/Files/Finance/1001.pdf [Accessed 30/04/2012].






Friday 27 April 2012

Mifumo ya uchumi wa kiIslam No 2

Kuna mifumo ya kiuchumi tofauti tofauti ambayo inatumiwa na bank za kiislam kwa ajili ya kufikia malengo yake mbalimbali kama vile kutoa huduma muhimu kwa wateja, kujipanua katika biashara zake na mengineyo. Makala hii itaelezea kwa mukhtasari mifumo shirikishi (Participatory), mifumo isiyokua shirikishi (Non-participatory) na mifumo upitishaji (Accessory).

Mfumo Shirikishi unatumika pale wahusika watakaposhirikiana katika biashara Fulani. Katika mfumo huu bank za kiislam zinatumia utaratibu unaojulikana Kama Mudaraba au musharaka (partnership). Mudaraba maana yake ni ushirikiano ambao mmoja ya washirika anatoa mtaji (capital) kama vile pesa, na mshirika mwengine anatoa juhudi zake kama vile elimu aliyonayo na kadhalika. Washirika wa aina hii watakubaliana kutokana na wanavyotaka ilimradi tu wasivunje sheria. Kisheria Makubaliano hayo yanatakiwa yawe kabla ya kuanza biashara husika, wakifanya hivyo basi watashirikiana pia katika faida itakayopatikana. kama itapatikana hasara basi yule aliyetoa mtaji (capital) ndie atakaepata hasara ya mtaji na yule aliyetoa juhudi atakua amepoteza kuhudi zake na wakati wake. Hapa yanaweza kujitokeza maswali mengi kama vile nini hukumu ya kisheria kama mmoja wa washirika hao atasababisha hasara kwa uzembe? hilo litazungumziwa kwa ufasaha zaidi hapo baadae.

Aina nyengine ya mfumo shirikishi ni musharaka (Profit and Loss Sharing) ambayo maana yake ni washirika katika biashara fulani watakaposhirikiana katika hali zote katika biashara yao, kwa mfano kila mshiriki atatoa mtaji (capital) na pia akatoa juhudi ktk kuendesha biashara yao isipokua kama kuna makubaliano maalumu. Washiriki hawa watagawana faida na hasara kiasi walivyoshirikiana na walivyokubaliana.

Mfumo usio shirikishi (Non-Participatory) ni mfumo ambao bank sio mshirika katika biashara husika, inamuachia mteja kufanya kila kitu yeye mwenyewe. Ktk mfumo huo aina za biashara zinazotumika ni kama vile Murabaha, salam na Istisnaa. Murabaha (cost plus profit financing) ni pale bank itakaponunua bidhaa kwa makubaliano na mteja na baadae bank ikamuuzia bidhaa hiyo wakati imeshaongeza faida yake. Moja ktk masharti ya murabaha ni pamoja na bank kutaja thamani iliyonunulia bidhaa hiyo.

Salam ni pale thamani ya bidhaa itakapotolewa wakati bidhaa hiyo haipo au haijawa tayari. Istisnaa ni kutoa thamani ya bidhaa zinazohusiana na viwanda(manufuctures) wakati bidhaa hizo hazijawa tayari. Ikumbukwe kwamba biashara aina ya Salam na Istisnaa zinatumika katika mazingira yasiyokua ya kawaida, kwani katika mazingira ya kawaida kinachouzwa kinatakiwa kiwepo wakati wa kuuziana. Lakini hata hivyo hili limeruhusiwa ndani ya Quraan, Hadithi na Ijmaa (consensus) kwa ajili ya kuwafanyia wepesi binadamu, pale tu yatakopokamilika masharti yafuatayo 1- Nilazima bei ya bidhaa ijulikane kwawahusika 2- wakati na mahali pakukabidhiana lazima pajulikane wakati wakufunga mikataba.

Upitishaji (Accessory or Miscellaneous) ni mfumo mwengine unaokubalika kiIslam. Katika mfumo huu bank inachukua malipo ya kazi yake tu, aina za biashara inayotumika katika mfumo huu ni kama Uwakala (agency), mfano wake ni pale bank inapochaguliwa kwa kazi maalumu kama vile uwakala wa kuuza au kununua zabuni fulani. Mara nyengine bank inatumika kama amanah (trustee) maana yake ni kwamba bank inachaguliwa kua msimamizi tu wa biashara au mkataba fulani.

Bank hiyo hiyo inaweza kufanya kazi ya uhamishaji tu hii inaitwa Hawalah (transfer) maana yake nipale bank inaposimamia uhamishaji wa umiliki kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyengine. Kwa maelezo zaidi fuatilia makala zijazo.

Wednesday 18 April 2012

Mifumo ya uchumi wa kiIslam no 1

Benki za kiIslam zinafanya kazi kama benki nyingine zisizokua za kiIslam, zinakubali akiba na zinatoa huduma zote za kibenk kwa kufuata misingi ya sheria ya kiIslam. Benki za kiIslam kama zilivyo benki za kawaida zinafanya biashara na zinaingiza faida ili ziendelee kuwepo na kuendesha shughuli zake. Zinafanya hivyo kwa kupokea amana (deposit) au bank inatoa mtaji kumpa mteja kwa matumaini ya kuingiza faida

Kwa hakika kinachofanyika ni kwamba bank inapokea amana (deposit) ambazo zinabadilika kua dhamana au madeni ya bank (liabilities), kwa upande mwengine amana hizo zinakua mtaji (funds) kwa upande wa wateja au kwa (management). Amana hizo zinafanyiwa biashara zenye faida, na faida inayopatikana inakua ni mtaji wa wenye akiba zao na itakayozidi inagawanywa kwa wateja kulingana na aina ya account zao. Kwa mfano kama account zao ni za uwekezaji, basi watashiriki ktk faida hiyo na kama sio za uwekezaji basi watabakiwa na mtaji wao. Faida nyingine inagawanywa kwa washiriki wengine ktk mtaji huo ambao wanajulikana kama (shareholders). Moja kati ya tofauti kubwa iliyopo kati ya bank za kiIslam na zisizokua za kiIslam ni uhakika wa kwamba kama ikipatika hasara basi inabidi igawanywe kwa wote walioshiriki kulingana na mfumo wa kiuchumi na uliotumika na aina ya account iliyofunguliwa.

Kwa ujumla tunaweza kusema kwamba bank za kiIslam zinakubali akiba kwa kutumia aina mbili za account. Ya kwanza ni account ambayo mteja anaweza kuchukua amana yake wakati wowote (on-demand deposit account) na ya pili ni account ya uwekezaji ambayo mteja anahifadhi pesa zake kwa malengo ya uwekezaji na kwa muda maalumu.

Ktk account ambayo mteja anaweza kuchukua pesa zake wakati wowote, bank hailazimiki kumpa mteja faida yoyote. Akiba ya namna hiyo kisheria, inachukua muelekeo wa kwamba mteja ameikopesha bank mkopo ambao unajulikana kama (interest- free loan) au amehifadhi,(wadia) au ameweka kama amana (trust).

Ni muhimu kukumbushana kwamba kama itakua mteja ameweka akiba yake kwa ajili ya kuhifadhi tuu au kama amana, bank haiwezi kuifanyia biashara akiba hiyo ispokua kwa ruhusa ya mteja mwenyewe, lakini bank italazimika kurudisha akiba ya mteja wa namna hiyo hata kama bank imepata hasara.

Ktk ile account ya uwekezaji bank inatakiwa itoe faida kama ikipata faida kitu ambacho kinaonekana ktk mazingira ya kawaida kama riba ambayo kwa sheria za kiIslam na sheria za dini nyingine hairuhusiwi kama tuivyoona ktk makala zilizotangulia. Labda unaweza ukajiuliza swali kwamba ni nini hasa kinachofanya faida hiyo iwe tofauti? jawabu ni kwamba, kwa hakika kinachofanya faida hiyo iwe tofauti na riba ni mifumo ambayo banki za kiislam inaitumia ktk kuizalisha akiba hiyo, mifumo ambayo inakubalika kisheria za kiislam na ambayo inajulikana kama mifumo ya uchumi wa kiislam (Islamic modes of finance).

Ktk makala zinazokuja tutaelezea kwa upana mifumo ya uchumi wa kiIslam