Thursday, 23 August 2012

Ijarah (Non-participatory mode) no 2

Tukiendelea kuzungumzia mifumo isiyokua shirikishi, ktk makala hii tutazungumzia Ijara (kukodi).

Ijarah ni neno la kiarabu lenye maana ya kukodi (lease), ktk sheria ya kiIslam kukodi na kukodisha kunaruhusiwa kisheria ‘akasema mmoja wa wanawake, "ewe baba yangu muajiri. Kwa hakika, mbora wa ulie muajiri ni mwenye nguvu muaminifu" (Quraan: 28:26 ).

kukodi kunatumiwa katika maana mbili tofauti, maana ya kwanza ni kukodi huduma kutoka kwa mtu, watu au shirika fulani kwa malipo maalum mliyopatana, na hapa ndipo tunapata muajiri na muajiriwa kama ifuatavyo, Yule anaetoa huduma anaitwa muajiriwa na Yule anaepata huduma anaitwa muajiri. Kwa mfano kama A anampa kazi B kama meneja mauzo kwa malipo maalum (lessor) kila mwezi,wiki,au mwaka, basi A anakua muajiri na B anakua muajiriwa. Kutokana na mfano huo tunajifunza ya kwamba unaweza kumuajiri mwalimu,mwanasheria,Daktari nakadhika. Pia mtu anaweza kua muajiri mahali fulani na muajiriwa mahala kwengineko na kuendelea.

Maana nyingine ya kukodi ni pale mtu, watu, kikundi, au shirika fulani wanapokodi kitu fulani kutoka kwa mtu, watu au shirika fulani na si kumkodi mtu mwenyewe, kwa mfano A kukodi nyumba ya B, au shamba ,gari ,tractor kwa muda maalum na kwa malipo maalum yanayoitwa kodi (lessor). Hapa tuweke wazi kidogo kua katika lugha ya Kiswahili malipo anayopewa mfanyakazi kwa huduma aliyoitoa yanaitwa mshahara kwa kua mara nyingi hutolewa kila mwezi, mwezi kwa kiarabu huitwa (shahri), na ndio maana kile kilichotolewa kila mwezi kikaitwa mshahara.

Aina hizi mbili za Ijarah (lease) zimezungumziwa na uIslam, na kila moja ina sheria zake maalum, lakini hii ya pili ndio inayotumika sana na benki zinazofuata sheria za kiIslam, na katika uwanja wa biashara na uekezaji kwa ujumla, na aina hii ya kukodisha ndio ambayo itazungumziwa kwa kirefu zaidi.

Sheria muhimu za kukodi (leasing)
1- Kukodi kuwe ni makubaliano au mikataba ambayo mmiliki wa kitu anahamisha matumizi ya kitu hicho kwa mtu mwengine kwa muda maalum na kwa malipo maalum.

2- Kitu kinachokodiswa kiwe na thamani ya matumizi,kwa maana hiyo vitu visivyo nathamani kimatumizi havikodiswi. Unaweza kukodisha gari,nyumba n.k.

3- Kitu kinachokodiswa kinabaki ni mali ya mmiliki ,na matumizi tu yatamilikiwa na mkodishaji. Vitu ambavyo havibakii na hutoweka vinapotumiwa kama mafuta, vinywaji, vyakula na kadhalika havikodishwi kisheria.

4- Katika mali inayokodiswa kama kutatokea uharibifu unaotokana na mkodishaji , basi atalipa na kama unamuhusu mmiliki basi atalipa mmiliki mwenyewe. Kwa mfano kodi za jengo zinazolipwa serikalini atalipa mwenye jengo na kodi za biashara zinazolipwa(TRA) atalipa mkodishaji.(isipokua kama kutakua na makubaliano maalum).

5- Muda wa kukodi ujulikane mwanzo na mwisho kabla ya kutumia mali iliyokodishwa.

6- Mali iliyokodishwa itumike kwa madhumuni yale tu yaliyoainishwa katika mkataba. Kama hayakuainishwa basi yawe katika matumizi ya kawaida na afahamishwe mmiliki matumizi hayo kabla.

7- Kama kutatokea uharibifu wowote wa kimakusudi katika mali iliyokodishwa basi mkodishaji atatakiwa kulipa alichoharibu.

8- Mali iliyokodiswa inakua katika hatari (risk) ya mmiliki katika kipindi chote cha ukodishwaji kwa maana uharibifu wowote utakaotokea nje ya uwezo wa mkodishaji utakua nijukumu la mmiliki.

9- Mali inayomilikiwa na wamiliki zaidi ya mmoja pia inaweza kukodiswa, mkodishaji atalipa kiasi cha kodi inayotakiwa kama kodi moja na kisha kodi itagawanwa kwa kiasi cha asilimia za wamiliki.

10- Mali inayomilikiwa na mtu zaidi ya mmoja haitakodiswa na mtu mmoja mmoja , isipokua kama kila mmoja anamiliki sehemu yake maalum, atakodisha sehemu yake tu.

11- Ni muhimu sana katika ukodishaji unaokubalika uwe unafahamika kwa njia ya uwazi kabisa kwa wahusika wote, kwa mfano kama A anamwambia B nakukodisha moja ya maduka yangu mawili, B akasema nimekubali, kukodi huku si sahihi mpaka aainishe duka gani kati ya hayo mawili analomkodisha?

Baadhi ya tofauti zilizopo kati ya kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam na kule kusikofuata sheria za kiIslam

Ktk kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam gharama za kukodisha zinaanza wakati bidhaa iliyokodishwa itakapofika kwa mteja, wakati ktk kukodisha kusikofuata sheria za kiIslam, gharama za kukodisha zinaanza haraka mkodishwaji atakapolipa gharama hata kabla ya kufikishiwa alichokikodisha.

Ktk kukodisha kunakofuata sheria za kiIslam hatari zote zinazohusiana na bidhaa zitabebwa na benki iwapo mkodishwaji hatasababisha madhara yoyote kwa makusudi au uzembe, wakati kukodisha kusikofuata sheria za kiislam hatari zote zinazohusiana na bidhaa zinabebwa na mteja bila kujali mazingira yaliyosababisha.

Kwa maelezo zaidi Fuatilia makala ijayo

No comments:

Post a Comment